Tuesday, 4 November 2014

WARIOBA ADHALILISHWA MDAHALO WA KATIBA

Katika mazingira ya kutatanisha, siku ya Jumapili vurugu zimekatisha mdahalo uliokuwa ukiendelea kujadili mchakato wa katiba mpya ya Tanzania huku baadhi ya watu wakipigwa na kujeruhiwa.

Mdahalo huo uliokuwa ukitangazwa moja kwa moja kupitia redio na televisheni ulivurugika kutokana na kundi la vijana wapatao 20 kuanza kumzomea aliyekuwa mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, alipokuwa akiwasilisha mada yake.

Vijana hao ambao haijajulikana walitokea wapi au walikuwa na ajenda gani waliinua mabango ya kupinga msimamo wa waliokuwa wakiendesha mdahalo na kusema rasimu ya katiba iliyopendekezwa inakidhi mahitaji yote na kusema hakuna haja ya mdahalo.

Jaji Warioba ambaye ni Waziri Mkuu mstaafu wa Tanzania alifanikiwa kutoka nje ya ukumbi ulipokuwa ukifanyika mdahalo huo mjini Dar Es Salaam, lakini wapo watu waliojeruhiwa kutokana na kurushwa viti na vitu vingine.

BBC iliwasiliana na Jaji Warioba apate kueleza yaliyotokea na kama yuko salama baada ya vurugu hizo, lakini aliomba radhi kwa kusema hayupo tayari kulizungumzia swala hilo.


No comments:

Post a Comment